Numbers 21:21-30

Kushindwa Kwa Sihoni Na Ogu

(Kumbukumbu 2:26–3:11)

21 aIsraeli akawatuma wajumbe kumwambia Sihoni mfalme wa Waamori:

22 b“Uturuhusu tupite katika nchi yako. Hatutageuka kando kwenda katika mashamba au mashamba ya mizabibu, ama kunywa maji kutoka kisima chochote. Tutasafiri kwenye njia kuu ya mfalme hata tutakapokuwa tumekwisha kupita katika nchi yako.”

23 cLakini Sihoni hakumruhusu Israeli apite katika nchi yake. Alilikutanisha jeshi lake lote, wakaondoka kwenda jangwani ili kupigana na Israeli. Alipofika huko Yahazi, akapigana na Israeli. 24 dHata hivyo, Israeli alimshinda kwa upanga na kuiteka ardhi yake kutoka Arnoni mpaka Yaboki, lakini ni hadi kufikia nchi ya Waamoni tu, kwa sababu mipaka yake ilikuwa imezungushwa ukuta. 25 eIsraeli akaiteka miji yote ya Waamori na kuikalia, pamoja na Heshboni na makazi yote yanayoizunguka. 26 fHeshboni ulikuwa mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alikuwa amepigana dhidi ya mfalme wa Moabu aliyetangulia na akawa amechukua ardhi yake yote mpaka Arnoni.

27Ndiyo sababu watunga mashairi husema:

“Njoo Heshboni na ujengwe tena;
mji wa Sihoni na ufanywe upya.

28 g“Moto uliwaka kutoka Heshboni,
mwali wa moto kutoka mji wa Sihoni.
Uliteketeza Ari ya Moabu,
raiya wa mahali pa Arnoni palipoinuka.
29 hOle wako, ee Moabu!
Umeharibiwa, enyi watu wa Kemoshi!
Amewatoa wanawe kuwa wakimbizi,
na binti zake kama mateka
kwa Mfalme Sihoni wa Waamori.

30 i“Lakini tumewashinda;
Heshboni umeharibiwa hadi Diboni.
Tumebomoa hadi kufikia Nofa,
ulioenea hadi Medeba.”
Copyright information for SwhNEN